DJM

JE UNAMFAHAMU NDEGE AINA YA KUNGURU

Na: Dotto Manumbu, DJM1

Hujambo na karibu msomaji wangu wa makala ya ndege aina ya kunguru, ili ufahamu mengi zaidi kuhusu aina mbalimbali za ndege wa aina hii, namna anavyoishi, chakula wanachokula na namna wanavyoishi, usichoke kusoma makala hii adhimu, karibu sana.


(Kunguru mwenye rangi mbili nyeusi na nyeupe akiwa amekaa katika mti maeneo ya mtaa wa Nchenga, Kata ya Nyegezi wilayani Nyamagana Jijini Mwanza- Picha na Dotto Manumbu)

Kunguru ni aina ya ndege wakubwa kiasi, wataalam wanasema ndege hawa wametokea katika familia ya  Corvidae. Hapa nchini Tanzania ndege hawa pia wapo katika maeneo mbalimbali kote nchini, wengi zaidi hupendelea kuonekana katika maeneo ya kando ya ziwa, katika masoko, makazi ya watu, mbuga za wanyama, mito, bahari, msituni na pengine huonekana katika machinjio ya mifugo mbalimbali ikiwa na maana kuwa ndege hawa hupendelea kula nyama pia.

Spishi nyingine ya ndege aina ya Kunguru katika mataifa mengine huitwa vinubi, ambao wanatokea mabara yote isipokuwa Antakitiki, mara nyingi ndege hawa huwa na spishi nyingi nyeusi pamoja na rangi nyeupe, kijivu au kahawia, ndege hawa wengine wana rangi mbalimbali wakiwepo wenye rangi ya buluu na pinki, ambapo wanaaminika kuwa na wanauwezo wa kuruka umbali mrefu angani kutoka usawa wa bahari na kumudu kusafiri umbali mrefu pasipo kuchoka.

(Kunguru wakiwa wanasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine mara baada ya kutoka kupata chakula katika soko la samaki kamanga lililopo Wilayani Ilemela Jijini Mwanza – Picha na Dotto Manumbu)

Ndege hawa hawabagui chakula, hula nusra kila kitu ya viumbe wakiwepo ndege wadogo, wadudu, mizoga ya mifugo au wanyama na ndege waliokufa, matunda, nafaka n.k, pia hulijenga tago lao kwa vijiti juu ya mti au jabali, wakati spishi nyingine huyajenga matago yao kwa makundi. 

(Kunguru akijitafutia chakula ambacho ni mzoga wa samaki mwambao wa ziwa Victoria wilayani Nyamagana Jijini Mwanza – Picha na Dotto Manumbu)

Kwa mujibu wa maelezo ya wazee maarufu katika Mkoa wa Mwanza wanaeleza kuwa ndege hawa ni moja ya ndege ambao wanasadikika kuishi umri mrefu zaidi kuliko ndege wengine, na ni mara chache sana kumkuta ndege huyu ameugua kwa ugonjwa wa aina yoyote, pia ndege hawa huaminika kuwa na siri kubwa hasa namna wanavyotaga mayai yao mpaka kutotolesha vifaranga na kwa mujibu wa historia, Kunguru jike hutaga mayai kuanzia 3 hadi 10.

Kunguru weusi wakipata chakula ambayo ni Samaki waliotupwa katika jalala la Buhongwa – Picha na Dotto Manumbu)

Baadhi ya Kunguru huonekana kuwa ni waharibifu kutokana na tabia yao ya kuvamia vyakula katika mashamba ya watu waliyolima ikiwepo kula mazao ya Mahindi, Karanga, Dengu, Njugu, Matunda yakiwepo Maembe na Mapela, hali hiyo hutokea mara nyingi wakati wa mavuno (kiangazi).

Pamoja na kwamba Kunguru ni ndege, lakini aina nyingine ya ndege hawa wanaweza kuiga sauti ya binadamu, lakini hawawezi kuongea kama ndege Kasuku alivyojaliwa na Mungu kuiga sauti mbalimbali zikiwepo sauti za binadamu, wanyama na miungurumo ya vyombo mbalimbali vya moto ikiwepo Gari, Pikipiki na mashine nyingine.

Hivyo, Kunguru wanaweza pia kufugwa na kufundishika kama walivyo ndege wengine wakiwepo Kasuku, Bata na Kuku, mara nyingi Kunguru wanaofundishika na kufikia hatua ya kuiga sauti ni wale wanaopatikana sehemu za bara la Asia ya Mashariki kwa sababu huchukuliwa kama alama ya bahati katika mataifa hayo.

Inawezekana ukaona ajabu, lakini kuna baadhi ya watu wanafuga Kunguru kama wanyama wa nyumbani, ndege hawa pia wana sifa kuwatambua watu na kuelewa kwamba hawa ni watu wabaya au hawa watu hawana madhara kwa maisha yao.

Tamaduni nyingi za kienyeji za kaskazi ya mbali, ndege hawa wamekuwa kama viumbe wa kiroho na wengine kuamini kuwa ni moja ya ndege ambao hutumiwa kishilikina. Lakini katika Afrika Waxhosa wa Afrika Kusini wanawachukulia ndege hawa kuwa ni ndege ambao wanabaraka kubwa katika maisha yao.

Kama viumbe wengine wote walivyo na tabia tofautitofauti, hivohivo na kwa Kunguru anatabia yake, Kunguru anamaamuzi ya haraka akihisi mazingira aliyopo si salama kwa usalama wa maisha yake, huruka na kuondoka eneo hilo haraka, aidha, ana macho yenye uwezo mkubwa wa kuona na kugundua kwa uharaka zaidi, ndege huyu pia amejizolea umaarufu wa kuwa na ujasiri mkubwa wa kujenga mahusiano na watu, hamwogopi binadamu tofauti na ilivyo kwa ndege wengine.

Kunguru jike rangi nyeusi akiwa katika mawindo yake kusaka chakula aina ya panzi katika vichaka vilivyopo maeneo ya mtaa wa Masha uliopo katika Kata ya nyegezi Jijini Mwanza – Picha na Dotto Manumbu)

Jambo jingine la kustajabisha, kwa mujibu wa maelezo ya wazee maarufu wa Mwanza akiwepo Mzee Jonas Siboka wanaoifahamu historia ya ndege hawa wameeleza kuwa, aina ya milio ya Kunguru mara nyingi huwa ni tata na migumu kuielewa kwa urahisi, milio yao hutofautiana kwa spishi tofauti. Pia Kunguru wanauwezo wa kusikia sauti ndogo sana ambazo binadamu hawezi kuzisikia. 

Aidha, kwa mujibu wa historia ya watu wa kale, Kunguru ni ndege ambaye anaaminika kuwa anasumu, hawezi kutumika kama kitoweo kama ilivyo kwa Kuku, Kware, Kanga, Njiwa, na ndege wengine. Baadhi ya makabila kama vile Wasukuma na Wanyamwezi humtumia ndege Kunguru kama nyenzo mojawapo ya ulinzi wa mazao yao yasiingiliwe kuliwa na ndege hao, wananchi wa makabila hayo huwaua kunguru na kuwasimika juu ya mti katikati ya shamba wakiwa na Imani kwamba endapo kunguru watafika eneo hilo basi wataogopa na kuondoka.

Baadhi ya makabila hapa nchini Tazania huamini kuwa Kunguru ni dawa inayoweza kutibu baadhi ya matatizo anayoyapata binadamu, na wengine huamini kuwa ndege hawa hutumika kwa masuala ya kishilikina.

Hadi kufikia hapo, Makala yetu kwa siku ya leo imefikia tamati nikusihi usikose mwendelezo wa makala hii kuhusu ndenge wa aina mbalimbali hapa ulimwenguni. Asante.






JE UNAMFAHAMU NDEGE AINA YA KUNGURU JE UNAMFAHAMU NDEGE AINA YA KUNGURU Reviewed by Manumbu blog on December 16, 2024 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.