DJM

MATUMIZI YA VYOO BORA YAMEONGEZEKA NCHINI TANZANIA

 






(Picha ikionesha Choo cha kisasa kilichopo Mtaa wa Nchenga Nyegezi ambacho kilitembelewa na Waziri Mhe. Jenista Mhagama kama mfano wa Choo bora. Picha na Dotto Manumbu, SAUT)


Na: Dotto Manumbu, SAUT


Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama (MB)  amesema Tanzania imekua na ongezeko kubwa la watu wanao tumia vyoo bora kutoka asilimia 43 mwaka 2020 hadi asilimia 84.8 mwaka 2024 ambapo ni hatua chanya ya kufikia lengo la 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya 2030 “Sustainable Development Goals”.


Waziri Mhagama alisema hayo Novemba 20, 2024 katika kikao cha Wizara kilichowahusisha wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi na viongozi wa mashirika mbalimbali wenye mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambapo katika tamko lake likionesha hali ya matumizi ya vyoo nchini ambapo mikoa inayoongoza kwa matumizi ya vyoo bora ni Dar es Salaam (98.5%), Ruvuma (92.1%) na Njombe (87.6%).


Aidha, Waziri Mhagama alisema licha ya kuwa tumepiga hatua kwenye kiashiria hicho bado kuna baadhi ya watu hawatumii vyoo ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 9.8 ya watu nchini hawana vyoo kabisa ambapo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.“Kwa mujibu wa taarifa hii asilimia 13.4 ya wakazi wa vijijini hawana vyoo kabisa. Tafsiri ya kiashiria hiki ni kwamba watu hawa ndiyo wanaojisaidia ovyo (Open defecation) vichakani na maeneo mengine ambayo sio rasmi. Hali hii inachangia kuwepo kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2024 jumla ya watu 749 waliougua na 16 kupoteza Maisha”. Alisema Waziri Mhagama.


Hata hivyo Waziri Mhagama alibainisha mikoa inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ni Katavi (24.3%), Simiyu (24.3%) na Manyara (22.3%) huku akiagiza Sekretatarieti za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kaya zote nchini zinakuwa na vyoo bora.




Picha ikionesha hali ya baadhi ya Kaya katika Mtaa wa Nchenga Nyegezi zikitumia vyoo vya shimo Picha na Dotto Manumbu, SAUT)


Waziri Mhagama ameielekeza Mikoa na Halmashauri kutekeleza kufanya ukaguzi kwenye kaya, sehemu za Jumuiya, maeneo ya biashara na Taasisi zote kwa kuhakikisha zinajenga na kutumia vyoo bora pia Kusimamia vyema Sheria ya Afya ya Jamii na Sheria Ndogo zinahusiana na ujenzi na matumizi ya choo bora kwenye ngazi ya Kaya, Taasisi na maeneo ya Jumuiya.


Aidha, Mhagama ameelekeza kuhakikisha zinasimamia vyema matumizi ya vyoo kwa wasafiri wawapo safarini kwa kuhakikisha mabasi yanasimama kwenye maeneo rasmi ikiwemo stendi za mabasi na vituo maalum pamoja na kupiga marufuku tabia ya wasafiri kujisaidia hovyo maarufu kama kuchimba dawa kwani ni aibu kwa Taifa na pia udhalilishaji wa utu.




MATUMIZI YA VYOO BORA YAMEONGEZEKA NCHINI TANZANIA MATUMIZI YA VYOO BORA YAMEONGEZEKA NCHINI TANZANIA Reviewed by Manumbu blog on November 21, 2024 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.